KITAIFA

YANGA SC YAMALIZANA NA MUDATHIR YAHYA

yanga

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/25, Yanga SC chini ya Kocha Mkuu, Miloud Hamdi wamekamilisha dili lao na kiungo kiraka Mudathir Yahya.

Mudathir Yahya mkataba wake ulikuwa umeisha mara baada ya msimu kufika ukingoni alikuwa kwenye mazungumzo na mabosi wa timu hiyo kuhusu kuongeza mkataba wake.

Ilikuwa inatajwa kuwa kiungo huyo alikuwa kwenye rada za Simba SC ambayo ilikuwa inafanya naye mazungumzo alipokuwa huru ili awe ndani ya kikosi chao.

Julai 22 2025, Yanga SC wamemtambulisha rasmi Mudathir kuwa ameongeza mkataba wa miaka miwili kuwa ndani ya kikosi hicho.

Ni 2025 mpaka 2027 Mudathir atakuwa kwenye majukumu yake katika kikosi cha Yanga SC kupambania kutimiza kazi ya kusaka ushindi kitaifa na kimataifa.

Msimu wa 2024/25 Mudathir alicheza jumla ya mechi 26 akikomba dakika 1,775 alitengeneza pasi nne za mabao na kufunga mabao manne hivyo alihusika kwenye mabao 7 kati ya 83 yaliyofungwa na Yanga SC.

Leave a Comment