Katika kumbukumbu za hivi karibuni za kuelekea dirisha la usajili, nukuu ya Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Jayrutty Investment Company Limited, CPA Joseph Rwegasira, inaendelea kuishi vichwani mwa Wanasimba.
Kauli yake ya kishujaa isemayo, “Kila mwaka tutasajili mchezaji mmoja ambaye Wanasimba wanamtaka, tutakuwa tunaambiwa na sisi tutakuwa tunamsajili,” ilikuwa ni zaidi ya ahadi; ilikuwa ni tangazo la vita ya kiuchumi na ushindani dhidi ya wapinzani wao wa jadi.
Rwegasira, kupitia kampuni yake, amejipambanua kama mdau mkubwa anayeamini katika kuwapa mashabiki kile wanachokihitaji ili kurejesha furaha ya Msimbazi kupitia usajili wa “Galacticos” wa kiwango cha juu.
Ahadi hii imeweka shinikizo chanya kwa bodi ya wakurugenzi ya Simba SC, kwani inafungua mlango wa usajili wa kidemokrasia ambapo sauti ya mwanachama inapewa kipaumbele kupitia uwekezaji wa Jayrutty.
Wakati huu ambapo vilabu kama Yanga vimekuwa vikishikilia mastaa wao kama Djigui Diarra kwa nguvu, ahadi ya CPA Rwegasira inatazamwa kama mbadala wa kuhakikisha Simba inapata fundi mmoja kila msimu ambaye atatikisa nchi. Mashabiki kwa sasa wanajiuliza, ni nani atakuwa “Mchezaji wa Wanasimba” kwa mwaka huu wa 2026? Je, ni winga machachari au mshambuliaji mwenye jina kubwa barani Afrika.










Leave a Reply