Kocha wa zamani wa Simba SC, Abdelhak Benchika, anaendelea kuonyesha umahiri wake nchini Algeria baada ya kuiongoza klabu yake ya USM Alger kukaa kileleni mwa Kundi A katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup).
Chini ya uongozi wake, USM Alger imefanikiwa kukusanya alama tisa (9) katika mechi tatu za kwanza, ikiwa na rekodi ya ushindi wa asilimia 100 baada ya hivi karibuni kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Djoliba AC. Benchika, akiwa na beki wake imara raia wa Cameroon, Chemalone, wanatuma salamu nzito kwa wapinzani wao kuwa msimu huu wamedhamiria kulitwaa kombe hilo kwa mara nyingine.
Uimara wa safu ya ulinzi inayoongozwa na Chemalone umekuwa nguzo muhimu kwa Benchika, ambapo timu hiyo imeruhusu mabao mawili tu huku ikifunga mabao sita katika hatua hii ya makundi.
Mafanikio haya yanazidi kuimarisha sifa ya kocha Benchika kama mmoja wa makocha bora barani Afrika katika michuano ya CAF, huku ushirikiano wake na Chemalone ukionekana kuwa na kemia ya kipekee inayowapa matumaini makubwa mashabiki wa Algeria. Kwa kasi hii waliyonayo, ni wazi kuwa USM Alger imejipanga vizuri kuvuka hatua ya makundi na kuelekea kwenye hatua za mtoano wakiwa na dhamira moja kuu: kubeba taji la ubingwa.










Leave a Reply