KIKOSI cha Simba SC kinachonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids asubuhi ya Septemba 17 2025 kimeanza safari ya kuelekea nchini Botswana kwa kupitia nchini Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone FC.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Jumamosi hii Septemba 20 huko Botswana kabla ya wiki moja kurudiana tena kwenye Uwanja wa Mkapa Jijini Dar es Salaam.
Simba imeondoka leo ikiwa ni saa chache zimeyeyuka tangu watoke kufungwa bao 1-0 katika Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga SC Septemba 16 2025 katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
Bao pekee la ushindi kwenye mchezo huo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayodhaminiwa na NBC msimu wa 2025/26 limefungwa na Pacome Zouzoua.
Miongoni mwa wachezaji wa Simba SC ambao wapo kwenye msafara huo ni Moussa Camara, Jonathan Sowah, Joshua Mutale, Seleman Mwalimu, Wilson Nangu.
Rekodi zinaonyesha kuwa inakuwa ni mara ya sita mfululizo Simba SC kupoteza mbele ya Yanga SC katika mechi za ushindani. Ikumbukwe kwamba msimu wa 2024/25 katika mechi mbili za ligi Simba SC ilifungwa nje ndani.