KUELEKEA kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa pili kati ya KenGold vs Simba SC Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, hesabu kali zinapingwa kwa timu zote mbili kuhitaji kusepa na pointi tatu muhimu.
Simba SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids walipokutana na KenGold Desemba 18 2024, ubao wa Uwanja wa KMC Complex ulisoma Simba SC 2-0 KenGold. Pointi tatu zilikuwa mali ya Simba SC.
Leo wanatarajiwa kukutana kwa mara nyingine kukamilisha dakika 180 za msako wa pointi sita ambapo zile za mwanzo ni Simba SC alisepa nazo baada ya dakika 90 kugota mwisho.
Seleman Matola, kocha msaidizi wa Simba SC amesema licha ya KenGold kushuka daraja wataingia kwa tahadhari kusaka pointi tatu muhimu.
“Tunatambua ni mchezo muhimu kwetu kupata matokeo mazuri licha ya kwamba KenGold ameshuka daraja bado tutaingia uwanjani kwa tahadhari kubwa kwa kuwa mchezo wetu huu ni muhimu na tunahitaji pointi tatu muhimu kama ambavyo wapinzani wetu wanahitaji pointi tatu.”
KenGold ipo nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 16 baada ya mechi 28, inawakaribisha Simba SC nafasi ya pili na pointi 72 baada ya mechi 27.