JIUNGE KWENYE WHATSAPP CHANNEL YA SIMULIZI ZA SAUTI ZA WAKUBWA TU BONYEZA HAPA KUJIUNGA
Klabu ya Yanga imesema haifanyi utani kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii, hivyo Kocha Mkuu, Romain Folz, amekuwa na ‘programu’ nne tofauti za maandalizi kuelekea mechi hiyo inayotarajiwa kupigwa, Septemba 16, mwaka huu, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kocha wa timu hiyo amekuwa na mazoezi ya gym, ufukweni, uwanjani na darasani kwa ajili ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ambao utakuwa unaashiria kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu mpya, Septemba 17, mwaka huu.
Kamwe amesema kocha Romain anataka kuendeleza rekodi za makocha wenzake, Miguel Gamondi na Miloud Hamdi, ambao walikuwa wakiisulubu Simba kila wanapokutana.
Alisema anataka kuendeleza rekodi ya Yanga kuifunga Simba, ambapo kama atafanikiwa itakuwa ni mara ya sita mfululizo kwa timu yao kuwafunga watani wao wa jadi.
“Timu inaendelea vizuri kumekuwa na programu tofauti tofauti za uwanjani, gym, ufukweni na darasani, huu ni mwendelezo wa maandalizi hasa kuelekea kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, ingawa tuna mchezo dhidi ya Bandari ya Kenya kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi.
“Mwalimu ni mpya na wasaidizi wake ni wapya, hilo linakupa picha kwamba wanataka kufanya vizuri. Mwalimu nimemwangalia ana vitu vingi, ana mbinu nyingi sana ambazo zitaanza kuonekana Wiki ya Mwananchi, Ngao ya Jamii na hata kwenye michezo ya kimataifa,” alisema Kamwe.