KITAIFA

Kocha Mpya wa Yanga 2025/2026: Siri Yafichuka Jangwani!

Kocha Mpya wa Yanga 2025/2026: Siri Yafichuka Jangwani!

KLABU ya Yanga SC imethibitisha kuwa tayari imepata Kocha Mpya wa Yanga kwa msimu wa 2025/2026, ambaye sasa ndiye anasimamia kikamilifu harakati za usajili kuelekea msimu mpya wa mashindano. Ingawa jina lake halijatangazwa rasmi, kocha huyo tayari yupo nchini na anaishi kwenye hoteli ya kifahari jijini Dar es Salaam akijifunza kikosi chake kwa undani kabla ya kuanza kazi rasmi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, kilichosalia kwa sasa ni kumalizia mchakato wa kuwaaga baadhi ya wachezaji waliomaliza mikataba yao, na mara baada ya hapo kocha mpya ataingia rasmi kazini kushiriki kikamilifu katika maandalizi ya msimu mpya.

Hivi sasa tunaanza kutoa barua za kuachana na baadhi ya wachezaji ambao hatutakuwa nao msimu ujao. Zoezi hilo likikamilika, tutaanza mazungumzo na wale tunaotaka kuwaongezea mikataba. Kocha mpya ndiye anasimamia kila hatua ya mchakato huu wa usajili,” alisema Kamwe

Yanga Yaingia Kwenye Historia, Malengo Yawekwa Kwa Kocha Mpya

Yanga imemaliza msimu wa 2024/2025 kwa mafanikio makubwa—ikiibuka mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya 31 na ya nne mfululizo, pamoja na kutwaa Kombe la Shirikisho la CRDB, Kombe la Toyota, Kombe la Muungano na Ngao ya Jamii. Pamoja na mafanikio haya, klabu hiyo inajiandaa kuweka rekodi mpya katika msimu ujao chini ya uongozi wa Kocha Mpya wa Yanga 2025/2026.

Kocha mpya amepewa malengo makubwa—kuchukua makombe yote ya ndani na kufika angalau nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambako Yanga itashiriki baada ya kuwa mabingwa wa Ligi Kuu.

“Yeye si tu kocha, bali ni mtaalamu wa soka la Afrika. Amepokea maagizo ya kuhakikisha timu inafanya vyema si tu nchini bali kimataifa,” kilisema chanzo kutoka ndani ya klabu.

Je, Ni Nani Kocha Mpya wa Yanga 2025/2026?

Ingawa jina bado halijatangazwa rasmi, vyanzo vya ndani vinaeleza kuwa kocha huyo huenda ni Julien Chevalier, raia wa Ufaransaaliyemaliza mkataba na ASEC Mimosas ya Ivory Coast. Chevalier ana uzoefu mkubwa barani Afrika na aliwahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Togo. Tangu mwaka 2019, amekuwa akihudumu katika ASEC, na sasa anatajwa kuwa ndiye atakayeongoza kikosi cha Yanga msimu ujao.

Pia jina la Rhulani Mokwena, raia wa Afrika Kusini na aliyewahi kuwa kocha wa Wydad Casablanca, liliwahi kutajwa, lakini taarifa zinaonyesha kuwa Yanga imeshafanya maamuzi rasmi na kocha aliyepitishwa ndiye anayesimamia usajili hivi sasa.

Kocha ameshatua nchini tangu wiki iliyopita na ameshakamilisha makubaliano na Yanga. Kwa sasa yupo hotelini akifuatilia kikosi, bado hajazungumza na wachezaji ila ameshaanza kuishauri klabu kuhusu usajili,” kilieleza chanzo cha uhakika.

Usajili wa Msimu Mpya Waanza Chini ya Kocha Mpya

Yanga imeamua kusimamisha kwa muda mpango wa kutumia ripoti ya benchi la ufundi lililopita ili kumpa kocha mpya nafasi ya kushiriki kikamilifu kwenye upangaji wa kikosi.

Hatujaanza usajili rasmi. Tuna majina ya wachezaji kutoka ripoti ya zamani, lakini si busara kusajili bila kocha mpya kushiriki. Tutashirikiana naye kwa karibu katika kila hatua,” aliongeza Kamwe.

Miongoni mwa wachezaji waliobakizwa ni kiungo tegemeo Khalid Aucho, ambaye amesaini mkataba mpya wa mwaka mmoja. Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kubakisha wachezaji mahiri kabla ya kuongeza sura mpya kikosini.

Maandalizi ya Msimu Mpya Kuanza Mwisho wa Julai

Timu ya Yanga inatarajiwa kuanza maandalizi ya msimu wa 2025/2026 mwishoni mwa mwezi Julai, na imepanga kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya moja ya timu kubwa kutoka Ligi Kuu England. Lengo ni kuimarisha kikosi mapema kabla ya kuanza mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.

Tunataka kocha awe sehemu ya kila uamuzi. Tukimtambulisha mapema huku usajili ukiendelea, tutakuwa na uwazi na mafanikio zaidi. Huu ndio mfumo wetu,” alisema Kamwe.

Leave a Comment