HASHEEM Ibwe, Ofisa Habari wa Klabu ya Azam FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, ametangaza nia ya kuwania ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, (CCM)
Ibwe amesema: “Salamu kwa Vijana wenzangu. Huu ni wakati wa kusimama imara, kuchukua nafasi na kuwa sehemu ya mabadiliko tunayoyataka kuyaona katika jamii zetu. Maendeleo hayaji kwa kusubiri, yanajengwa na watu wenye maono, bidii, na moyo wa kujitolea. Na hakuna kikundi chenye nguvu, maarifa, na ari kubwa kama sisi vijana.
“Tuna nguvu. Tuna uwezo. Tuna wajibu. Tushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ikiwemo suala la uongozi kuchora dira yetu wenyewe. Kama si sisi, ni nani? Kama si sasa, ni lini?
“Natangaza rasmi nia yangu thabiti ya kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi, (CCM) ya kupeperusha bendera ya chama jimbo la Mwanga, Kilimanjaro mkoa na wilaya ninayotoka.
“Tuungane kwa pamoja, tuamke, na tuijenge Tanzania mpya yenye maendeleo ya kweli yanayoanzia kwa vijana.”