JIUNGE KWENYE WHATSAPP CHANNEL YA SIMULIZI ZA SAUTI ZA WAKUBWA TU BONYEZA HAPA KUJIUNGA
Memphis Depay amekuwa rasmi mfungaji bora wa muda wote wa Uholanzi. Alifikia hatua hii muhimu wiki hii Septemba 7, 2025, wakati wa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA dhidi ya Lithuania, ambapo alifunga mara mbili na kuiongoza timu yake kushinda 3-2.
Mabao hayo yalimfanya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31 kuvuka rekodi ya awali ya Robin van Persie ya mabao 50 katika timu ya taifa.
Bao la kwanza la Depay katika mechi hiyo, dakika ya 11 kutoka kwa krosi ya Cody Gakpo, lilikua bao lake la 51 la kimataifa, na kuvunja rekodi hiyo.
Kisha akaongeza jingine katika dakika ya 63 kwa kichwa chenye nguvu akiunganisha krosi ya Denzel Dumfries, na kuihakikishia Uholanzi ushindi huo na kufikisha jumla ya mabao 52 katika mechi 104 alizocheza.
Uholanzi kwa sasa wako kileleni mwa Kundi G katika mchujo wakiwa na pointi 10 kutokana na mechi nne.
Depay, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Corinthians ya Brazil, amekuwa na safari ya ajabu ya kikazi, ikiwa ni pamoja na kucheza PSV, Manchester United, Lyon, Barcelona, na Atletico Madrid.
Alianza kuichezea Uholanzi mwaka wa 2013 na kufunga bao lake la kwanza la kimataifa kwenye Kombe la Dunia la 2014.