KLABU kongwe nchini, Simba na Yanga, zimetembeza panga kwa upande wa wachezaji wa kimataifa kuelekea msimu mpya, huku zikilenga kuboresha vikosi vyao zaidi kwa ajili ya malengo makubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imefahamika.
Simba na Yanga zipo kwenye harakati za kuviboresha vikosi vyao kwa ajili ya mashindano msimu ujao, zikilenga zaidi Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo inatajwa kuwa vitaacha kadhaa wa kigeni.
SIMBA
Imeelezwa kuwa Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, katika wachezaji wa kigeni waliopo kwa sasa, amependekeza kubakiwa na saba tu, majina ni Steven Mukwala na Joshua Mutale, yakitajwa kutakiwa kusalia Msimbazi kwa msimu ujao wa mashindano.
Habari kutoka ndani ya Klabu ya Simba, zinasema japo wachezaji hao wawili awali walitajwa kuwa huenda wasingekuwapo msimu ujao, Mukwala akitajwa kupata ofa kutoka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na Mutale kuwa na kiwango cha kupanda na kushuka, lakini Faldu amependekeza wasalie kwani anawahitaji.
Wachezaji wengine ambao Fadlu anahitaji kufanya nao kazi akiwa amepewa kazi ya kutwaa taji angalau moja la ndani, hasa Ligi Kuu Tanzania Bara na kufika angalau nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ni Jean Charles Ahoua na Chamou Karaboue, wote raia wa Ivory Coast, Elie Mpanzu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Moussa Camara kutoka Guinea na Valentine Nouma, raia wa Burkina Faso.
Wachezaji hao wote walisajiliwa na kuichezea Simba kwa msimu mmoja tu.
Taarifa zinaeleza kuwa, Mukwala raia wa Uganda, aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Asante Kotoko ya Ghana na kusaini mkataba wa mwaka mmoja, yupo mbioni kuongeza mkataba mwingine baada ya Kocha Fadlu kuwaambia mabosi wa klabu hiyo kuwa wafanye juu chini asiondoke.
“Budo naye yupo sana, kocha amesema ni mchezaji mzuri sana, kwa sababu safari hii ataanza naye tena kwenye ‘pre season’ atamtengeneza maeneo ambayo ana matatizo, ambalo ni stamina ndiyo inayomtatiza, hakuwa na msimu mzuri wa maandalizi, lakini amesema kama akipata utimamu wa mwili atakuwa tishio,” alisema mtoa taarifa toka ndani ya Simba.
Wachezaji waliosalia ambao hawakutajwa na kocha kuwa ataendelea nao ni Che Fondoh Malone na Leonel Ateba, wote raia wa Cameroon, Debora Fernandes Mavambo, Augustine Okejepha raia wa Nigeria na Fabrice Ngoma raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambaye tayari ameshaaga mashabiki wa timu hiyo, taarifa zikisema kuwa anakwenda kujiunga na Klabu ya Hassania Union Sport Agadir ya Morocco.
“Kwa maana hiyo Simba itasajili wachezaji watano wa kigeni kuelekea msimu ujao, hao watano ni wachezaji wa daraja la juu, nia ni kukibadili kabisa kikosi kuwa imara, unajua timu inaweza kubadilika kabisa na kuwa imara hata ikiwa na wachezaji watatu tu wa maana.
“Ikumbukwe wakati huo hapa nchini kanuni ilikuwa inaruhusu watatu tu wa kigeni, sisi tuliwasajili, Emmanuel Okwi, Joseph Owino na Patrick Ochan, wote kutoka Uganda mwanzoni mwa miaka ya 2010/11, wakaungana na kina Mbwana Samatta hapa, ilibadilika kabisa na kuwa tishio na ile ilikuwa ndiyo safari ya timu hii kutoka kuwa Tanzania kwenda Afrika Mashariki na kati na sasa Afrika nzima,” kilisema chanzo chetu.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema kwa sasa viongozi wa Simba wapo kwenye hekaheka za usajili na muda wowote wataanza ratiba yao ya miaka yote ya kuanza kuaga mchezaji mmoja mmoja ambao wataachana nao, kabla ya kuanza kutaja majina ya wachezaji wapya watano wa kigeni, lakini pia baadhi Watanzania.
“Mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi, tatizo ni kwamba msimu uliopita tulitengeneza kikosi ambacho kimefanya vizuri sana, kimevunja rekodi nyingi za misimu minne, kiasi kila mmoja akasahau kuwa tulikuwa tunatengeneza kwani kiligeuka kuwa cha ushindani, kimekosa makombe dakika za mwisho kabisa, sasa tunakiongezea nguvu mara dufu,” alisema Ahmed.
YANGA
Kwa upande wa Yanga inaelezwa itaachana na wachezaji wanne wa kigeni, huku Duke Abuya akiwagawa viongozi.
Wachezaji ambao wanatajwa kuwa huenda wakapewa mkono wa kwaheri hivi karibuni ni Yao Kouassi, Jonathan Ikangalombo, Clatous Chama na Kennedy Musonda, huku kiwango cha hali ya juu kilichooneshwa na kiungo raia wa Kenya, Abuya, katika michezo ya hivi karibuni kikifanya viongozi kugawanyika na kusitisha kufanya maamuzi.
“Msimu ulioisha umekuwa poa sana, katika kikosi cha Yanga unatakiwa kila muda uwe kwenye kiwango cha kushindana, sina la kusema nadhani msimu ujao mtaweza kuniona kwa sababu mimi bado ni mchezaji wa Yanga,” alisema Duke, aliyesajiliwa kipindi cha dirisha dogo akitokea Singida Black Stars.
Chanzo kimesema kuwa nafasi ya Duke, ilishapewa mtu wa kuiziba ambaye ni Mohamed Doumbia (26), raia wa Ivori Coast, aliyekuwa akiichezea FC Slovan Liberec ya Jamhuri ya Czech, lakini kwa sasa anaichezea Majestic ya Burkina Faso.
Hata hivyo, viongozi wa Yanga wameamua vyovyote iwavyo, abaki au aachwe, lakini mchezaji huyo mpya lazima asajiliwe.
Kwa upande wa Chama, raia wa Zambia chanzo chetu kimesema nafasi yake itachukuliwa na Celestin Ecua, raia wa Ivory Coast, anacheza eneo la namba 10, mshambuaji msaidizi, aliyefunga mabao 15 na ‘asisti’ 12, kwenye michezo yote aliyocheza msimu huu, akiwa na kikosi cha Ivory Coast.
“Yanga haisajili kwa mihemko, au kushindana na mtu, kila usajili unaona mtu anasajiliwa kwenda kuziba nafasi ya mtu fulani, safari hii wameamua kuongeza wachezaji wenye viwango vya juu zaidi kwa sababu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tunataka kufanya vizuri,” alisema mtoa taarifa ndani ya klabu hiyo.
Musonda ambaye mkataba wake umekwisha, tayari ametangazwa kujiunga na Klabu ya Daraja la Pili ya Israel, Hapoel Ramat Gan Givatayim FC, kutokana na kushindwa kupata nafasi mbele ya Prince Dube na Clement Mzize.
Yanga inasaka straika mwingine wa kiwango cha juu, ili kuja kusaidiana na Dube, kwani huenda ikamkosa Mzize msimu ujao ambaye amekuwa na ofa nyingi kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.
Ikangalombo, aliyesajiliwa kipindi cha dirisha dogo akitokea AS Vita Club, ameshindwa kuwashawishi viongozi, wanachama pamoja na mashabiki wa Yanga, kutokana na kiwango chake kutoridhisha, hivyo taarifa zinaeleza kuwa alitaka kutolewa kwa mkopo lakini, wanaomsimamia wamekataa kata kata wakisema badala ya kufanya hivyo, wavunje mkataba ili achague mwenyewe timu ya kwenda kuichezea.
Aidha, viongozi wa Yanga bado wamekuwa na imani na Kouassi, ambaye amekuwa majeruhi wa muda mrefu, wakitaka kumpeleka akacheze nje ya Tanzania kwa mkopo kabla ya kumrejesha dirisha dogo la usajili, huku nafasi yake akitafutwa mtu mwingine ambaye ni Ibrahim Keita wa TP Mazembe, raia wa Mauritania, ingawa klabu zingine ikiwapo Esperance ya Tunisia nayo imetia nia kumwania.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amewaambia wanachama na mashabiki wa Yanga kuwa chochote kitakachofanya au kuamriwa kitakuwa ni kwa maslahi mapana ya klabu, huku akisema linapokuja suala la usajili mara nyingi hawakurupuki kuacha na kusajili ovyo, kwani huwa makini sana.
“Ukiona mchezaji kaondoka ujue hatumhitaji, nadhani wiki ijayo tutakuwa tumewapa barua wote wale ambao hatuwahitaji, wale tunaotaka kuwaongeza mikataba tutaanza kuzungumza nao, usajili unaendelea chini ya kocha wetu mpya,” alisema Kamwe.