UONGOZI wa Simba SC umebainisha kwamba utafanya kweli kwenye usajili hivyo mashabiki wasiwe na presha mipango inaendelea.
Ikumbukwe kwamba timu hiyo msimu wa 2024/25 ilikosa mataji yote iliyokuwa inayapambania jambo ambalo linawafanya waje na hasira zaidi. Miongoni mwa wachezaji ambao wanatajwa kuwa katika rada za Simba SC ni Feisal Salum wa Azam FC.
Kwenye ligi ilimaliza ikiwa nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 30. Katika dakika 2,700 uwanjani ushindi ulikuwa katika mechi 25, sare tatu na ilipoteza mechi mbili. Mechi zote mbili ambazo ni dakika 180 ilikuwa dhidi ya Yanga SC ambao ni mabingwa wa ligi inayodhaminiwa na NBC.
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba SC 0-1 Yanga SC. Mzunguko wa pili ilikuwa Yanga SC 2-0 Simba SC. Ni mabao matatu Yanga SC walifunga mbele ya Simba SC iliyokosa kuvuna pointi kwenye Kariakoo Dabi.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC ameweka wazi kuwa kuna kazi kubwa ambayo inafanywa na viongozi mashabiki wawe na subira.
“Viongozi wanafanya kazi kubwa kwa ajili ya kufanya usajili makini na mazuri hivyo mashabiki wawe na subira tutakuwa na furaha hakika.”