Home KITAIFA RC MAKALLA AKAGUA UWANJA WA AFCON ARUSHA

RC MAKALLA AKAGUA UWANJA WA AFCON ARUSHA

78
0
Makalla

JIUNGE KWENYE WHATSAPP CHANNEL YA SIMULIZI ZA SAUTI ZA WAKUBWA TU BONYEZA HAPA KUJIUNGA

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Amos Gabriel Makalla leo Ijumaa Septemba 05, 2025 ametembea na kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu utakaotumika kwenye mashindano ya Mataifa ya Afrika ya AFCON mwaka 2027 unaojengwa na serikali kwa gharama ya Shilingi Bilioni 340, kwenye Kata ya Olmot Jijini Arusha.

Ukaguzi huo umefanyika baada ya kikao kazi kilichofanyika kikihusisha wakuu wa idara na mamlaka zinazohusika na miundombinu ya huduma za Maji, nishati, barabara na mawasiliano katika uwanja huo, wakiazimia kuteua Kikosi kazi cha wataalamu wa sekta hizo chini ya mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ambao watakuwa uwanjani hapo muda wote kushughulikia uwekaji wa miundombinu hiyo chini ya Mpango mkakati wa dharura.

“Kama Mkoa wa Arusha tunajivunia utalii, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya mambo mawili Royal Tour, ametangaza utalii na anatuletea Utalii wa michezo (sport tourism) na uwepo wa uwanja huu utaongeza mzunguko wa pesa utakaochochea ukuaji wa biashara na uchumi wa mtu mmoja mmoja na mkoa kwa ujumla, hivyo tunamuhakikisha Mhe. Rais kwamba tutamuwakilisha vyema, tutasimamia ukamilishaji wa uwanja huu ili kuhakikisha malengo aliyotarajia yanatimia na mkandarasi ametuhakikishia kwamba utakamilika kama ilivyopangwa Julai 2026.” Amesema Mhe. Makalla.

Aidha Mhe. Makalla amesisitiza kuwa uwanja ni mkubwa na wa kisasa wenye kukidhi viwango vya Shirikisho la soka barani Afrika CAF, akisema maamuzi haya ya Rais Samia ya kutumia mapato ya serikali kuujenga uwanja huo yanakwenda kuipa heshima Tanzania na kuwapa fursa wananchi wa Arusha na watanzania kwa ujumla kuweza kushuhudia mashindano hayo nchini mwao, yakifanyika kwa ushirikiano wa Mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda.

Hata hivyo Mwakilishi wa mkandarasi anayetekeleza mradi huo China Railway Construction ya nchini China Mhandisi Denice Benito Mtemi amesema ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 60 ukitarajiwa kujumuisha nyasi asili kwenye sehemu ya kuchezea.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here