MSHAMBULIAJI namba moja kwa wazawa wenye mabao mengi msimu wa 2024/25 Clement Mzize bado ana mkataba na Yanga SC kuelekea msimu wa 2025/26.
Mzize amekuwa akitajwa kuwa katika rada za timu mbalimbali ambapo kuna timu moja kutoka Tunisia inatajwa kuweka dau kubwa mezani kupata saini yake kwa ajili ya changamoto mpya.
Rekodi zinaonyesha kuwa msimu wa 2024/25 Mzize alifunga jumla ya mabao 14 kwenye ligi ambapo Yanga SC walitwaa ubingwa na safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ilifunga jumla ya mabao 83 ikiwa ni timu iliyofunga mabao mengi.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga SC amebainisha kuwa Mzize ni mchezaji wa Yanga SC na kuna ofa ambazo zipo ikiwa zitajibiwa taarifa itatolewa kuhusu mchezaji huyo.
“Clement Mzize bado ana mkataba na Yanga SC hivyo kwa sasa ni mali yetu mashabiki ninapenda kuwahakikishia kuwa mchezaji tupo naye hajaondoka. Kuhusu ofa kuna ofa zaidi ya mbili kwa mchezaji wetu hizo zinafanyiwa kazi.
“Makubaliano yakifika taarifa itatolewa kwa kuwa mchezaji bado yupo hivyo hakuna tatizo kuhusu wengine kusema hivi na vile, viongozi tupo na masuala ya kimkataba yanatatuliwa kwa mkataba.”