YANGA KAMILI KUWAVAA SINGIDA FOUNTAIN GATE
MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa wapo tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Fountain Gate unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Gamondi amebainisha kuwa wanatambua ugumu uliopo kutokana na kuwa na mechi mfululizo lakini watafanya kazi kubwa kupata matokeo mazuri uwanjani.
“Maandalizi ni ya kawaida kwasababu tumetoka kucheza juzi na tunajua mchezo wa kesho utakuwa mgumu lakini tumejiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri.
“Falsafa ya kwanza ya Yanga ni timu na siyo mchezaji mmoja mmoja, wenyewe mmekuwa mashahidi michezo yetu iliyopita tulikuwa na majeruhi lakini kila Mchezaji aliyepata nafasi ya kucheza amefanya kazi yake vizuri.
“Napenda pia kuwapongeza mashabiki wetu kwa kazi nzuri wanayoifanya kila mahali tunapokwenda kucheza na nilishangaa mashabiki wetu hapa Mwanza kwenye mchezo tuliocheza hapa dhidi ya Geita, walikuwa wanashangilia kwa nguvu muda wote wa mchezo ilikuwa ni kama niko Amerika Kusini na najua watakuja kwa wingi kutupa sapoti,”.