VITA YA KUSAKA POINT TATU MECHI YA SIMBA VS JKT TANZANIA NI BALAA

Mchezo mkali wa Ligi Kuu NBC msimu wa 2025/26 unaendelea kupamba moto, ambapo timu ya JKT Tanzania inatarajiwa kuikaribisha Simba SC katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo mnamo Novemba 8, 2025.

Katika mchezo wa mwisho kukutana msimu uliopita, Simba SC ilivuna pointi tatu ugenini baada ya kushinda kwa bao 1-0, bao lililofungwa na Fabrince Ngoma ambaye kwa sasa hayupo kwenye kikosi cha Simba msimu huu. Hivyo, mchezo wa safari hii unatarajiwa kuwa na upeo tofauti kutokana na mabadiliko ya vikosi na mbinu za makocha.

Akizungumza kuelekea mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Simba SC, Seleman Matola, amesema maandalizi wameyafanya kikamilifu na wanatambua ugumu wa pambano hilo kutokana na uimara wa wapinzani wao.

“Tunatambua kwamba mchezo utakuwa mgumu lakini tupo tayari. Kikubwa ni kuona tunapata pointi tatu muhimu,” amesema Matola.

Kwa upande wa mwenendo wa ligi, JKT Tanzania hadi sasa ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 7 baada ya mechi tano, ikishinda mchezo mmoja na kupata sare katika mechi nne. Hali hii inaonesha kuwa ni timu inayocheza kwa nidhamu na ugumu wa kukubali kupoteza.

Simba SC inashika nafasi ya saba ikiwa na pointi 6 baada ya mechi mbili, ambazo zote ilicheza nyumbani na kuibuka na ushindi. Mchezo huu utakuwa wao wa kwanza ugenini msimu huu, jambo linaloongeza hamasa ya kuona namna watakavyojimudu mbali na nyumbani.

Mashabiki wa soka nchini wanatarajia mchezo wenye kasi, ushindani na mbinu, hasa katika eneo la kiungo ambapo timu zote zimeonesha uimara.