Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC imeeleza kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watu kuitisha mkutano usio rasmi na kutoa maneno ya kashfa pamoja na kauli zisizo na staha dhidi ya mwekezaji wa klabu hiyo, Ndugu Mohammed G. Dewji.
Klabu imesisitiza kuwa vitendo hivyo havikubaliki na haitatabari wala kuvumilia mtu yeyote atakayeharibu taswira ya klabu kwa namna yoyote ile, huku wakitoa pole rasmi kwa Ndugu Dewji kutokana na usumbufu huo.
Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Simba umeliandikia Jeshi la Polisi ili kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote waliohusika katika mkutano huo ama “kula njama,” kwa lengo la kuwafikisha kwenye vyombo vya dola kwa makosa ya jinai.
Aidha, klabu imetoa onyo kali kuhusu matumizi haramu ya nembo za wadhamini wao yaliyofanyika katika mkutano huo usio rasmi, ikisisitiza kuwa itachukua hatua za kisheria kulinda haki za wadhamini wake.