Manchester United yaishtaki Morocco FIFA kisa Noussair Mazraoui

Morocco

Manchester United imeripotiwa kuwasilisha malalamiko kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kufuatia uamuzi wa Shirikisho la Soka la Morocco kumzuia beki wao, Noussair Mazraoui, kucheza katika mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Bournemouth.

Mashetani Wekundu waliamini kuwa Mazraoui alikuwa bado anastahili kucheza mechi hiyo kwa mujibu wa kanuni za FIFA zinazohusu kuachiliwa kwa wachezaji wanaoshiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Kwa mujibu wa kanuni hizo, mchezaji anapaswa kuachiliwa siku saba kabla ya mechi ya ufunguzi ya taifa lake, huku kipindi rasmi cha kuachiliwa kikianza Desemba 15, siku ambayo Manchester United walipangwa kucheza dhidi ya Bournemouth.

Baada ya Morocco kukataa ombi la awali la United, uongozi wa klabu hiyo uliamua kuwasilisha suala hilo FIFA, wakitarajia kanuni zingewapa nafasi ya kumbakiza mchezaji huyo kwa mechi hiyo muhimu.

Hata hivyo, matumaini ya United yalikatishwa haraka baada ya FIFA kuunga mkono msimamo wa Shirikisho la Soka la Morocco, ikieleza wazi tarehe ya kuanza kwa kipindi cha kuachiliwa kwa wachezaji na hivyo kuiacha United bila nafasi ya kubadilisha uamuzi huo.

Morocco ilionekana kuweka kipaumbele kwenye maandalizi ya kikosi chake na kambi ya mazoezi kuelekea AFCON, badala ya kuruhusu mchezaji huyo kushiriki mechi ya Ligi Kuu ya England.

Pamoja na yote hayo, hakuna lawama zilizomlenga Mazraoui mwenyewe, kwani beki huyo alikuwa akiendelea na mazoezi na Manchester United kwa wiki nzima kabla ya kuondoka Jumapili jioni kwenda kujiunga na kikosi cha taifa cha Morocco.