KOCHA wa Klabu ya Simba, Steve Barker, amesema kuwa mchezo wa kesho dhidi ya Muembe Makumbi katika Kombe la Mapinduzi ni muhimu kwa maandalizi ya kikosi chake.
Amesema licha ya kuelewa kuwa mashindano hayo yana uzito mkubwa kama ilivyo kwa mashindano ya kimataifa yanayowakabili baadaye.
Barker amesema lengo kubwa la Simba katika michuano hiyo ni kuwapa wachezaji muda wa kucheza na kurejesha ubora wao wa ushindani baada ya mapumziko, huku akitumia fursa hiyo kujaribu mbinu mbalimbali kabla ya mechi ngumu zijazo.
Barker ameongeza kuwa ingawa Kombe la Mapinduzi kipaumbele kikubwa kwa Simba, bado anaamini ni jukwaa zuri la kuwakagua wachezaji wake na kuona kiwango chao cha utayari, hasa wale waliokuwa nje ya uwanja kwa muda kutokana na majeraha au majukumu mengine.
Kocha huyo amesema anafurahi kuona ari na morali ya wachezaji wake ipo juu, kila mchezaji anaonesha njaa ya ushindani na dhamira ya kupigania nafasi ndani ya kikosi cha kwanza kuelekea mechi muhimu za Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League).
“Lengo letu si tu kushinda mechi, bali kuona namna wachezaji wanavyotekeleza maelekezo ya kiufundi ndani ya uwanja, kujenga maelewano na kuongeza kasi ya timu,” amesema Barker.
Akizungumzia mchezo dhidi ya Muembe Makumbi, Barker amesema ana heshima kubwa kwa mpinzani wao na ameandaa kikosi chake kucheza kwa umakini mkubwa.
Amesema katika soka hakuna mechi nyepesi na kila mpinzani anapaswa kuchukuliwa kwa uzito unaostahili.
Simba inatarajia kushuka dimbani kesho ikiwa na dhamira ya kuonyesha ubora wake, huku mashabiki wakitarajia kuona mabadiliko chanya katika uchezaji wa timu yao kuelekea safari ya Ligi ya Mabingwa Afrika.









Leave a Reply