UONGOZI wa klabu ya Simba umeweka wazi kuwa uamuzi wa kumuongezea mkataba kiungo Elie Mpanzu umetokana na tathmini ya kina ya benchi la ufundi, iliyothibitisha umuhimu wake kuendelea kusalia kikosini kwa msimu ujao.
Benchi hilo la ufundi, linaloongozwa na Kocha Mkuu Steve Barker, liliridhishwa na mchango wa mchezaji huyo na kupendekeza aongezewe mkataba wa kuendelea kuitumikia timu hiyo kwa misimu miwili zaidi.
Kutokana na mapendekezo hayo, Mpanzu amesaini mkataba mpya wa miaka miwili utakaomuweka ndani ya Simba hadi mwaka 2028, baada ya ule wa awali kufikia ukingoni.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesisitiza kuwa kuongeza mkataba wa mchezaji huyo hakukutokana na presha ya ushindani kutoka kwa wapinzani wao, bali ni maamuzi ya kiufundi yaliyofanywa kwa maslahi ya timu.
Alibainisha kuwa licha ya kuwapo kwa jitihada kutoka kwa wapinzani wao wakuu kumshawishi nyota huyo, Mpanzu aliamua kubaki Simba baada ya kuridhishwa na mwelekeo wa klabu hiyo.
“Mapendekezo ya benchi la ufundi yalituongoza kufanya maamuzi haya. Tulimuita mchezaji, tukazungumza naye na hatimaye akakubali kuendelea kubaki ndani ya Simba,” amesema Ahmed.
