Mambo yamezidi kuwa magumu kwa Real Madrid katika mbio za kuwania ubingwa wa La Liga, baada ya kupoteza alama muhimu kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Real Betis ugenini, katika dimba la La Cartuja jijini Sevilla.
Real Madrid walianza vyema mchezo huo, wakitangulia kupata bao kupitia Vinicius Junior mapema katika kipindi cha kwanza, bao lililoashiria matumaini ya kuondoka na pointi tatu muhimu.
Hata hivyo, matumaini hayo yalififia katika dakika za mwisho kabisa za mchezo, pale Hector Bellerin alipofunga bao la kusawazisha kwa upande wa Real Betis katika dakika za nyongeza.
Matokeo hayo yanaifanya Real Madrid kubaki nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, wakiwa nyuma kwa alama nane dhidi ya vinara Barcelona, ambao bado wana mchezo mmoja mkononi. Hali hii inaongeza presha kubwa kwa Madrid, ambao sasa wanahitaji ushindi mfululizo huku wakitegemea wapinzani wao kudondosha alama ili kufufua matumaini ya ubingwa.
Kwa sasa, mbio za ubingwa zinaonekana kuwa ngumu zaidi kwa Real Madrid, huku Barcelona wakionekana kuwa na kasi na uthabiti wa kuwapeleka karibu zaidi na taji hilo.
