Klabu ya Simba SC imezidi kudhihirisha ukubwa wake katika nyanja ya kidijitali baada ya kufanikiwa kuingia kwenye orodha ya timu 20 bora duniani zenye wafuasi wengi zaidi kupitia mtandao wa WhatsApp. Kwa mujibu wa takwimu za Global Football Digital Benchmark 2026, Simba SC inashika nafasi ya 19 ikiwa na wafuasi zaidi ya milioni 2.4, ikiwa ndiyo klabu pekee kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuingia katika orodha hiyo ya dhahabu. Mafanikio haya yanaonyesha nguvu ya mashabiki wa “Wekundu wa Msimbazi” katika kufuatilia habari za timu yao kupitia mifumo ya kisasa ya kijamii.
Katika orodha hiyo, miamba ya Hispania, Real Madrid, inaongoza ikiwa na wafuasi zaidi ya milioni 67, ikifuatiwa na FC Barcelona yenye wafuasi milioni 54. Kwa upande wa Afrika, Simba SC inachuana vikali na timu kama Al Ahly ya Misri (milioni 3.4) na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini (milioni 2). Hii ni ishara tosha kuwa soka la Tanzania limeanza kupata ushawishi mkubwa duniani, huku Simba SC ikitumika kama kioo cha mafanikio ya kidijitali kwa vilabu vingine barani Afrika.
