Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, ameelezea kutoridhishwa kwake na kiwango kilichoonyeshwa na vijana wake katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Muungano 2026 dhidi ya Young Africans (Yanga SC) uliopigwa leo Aprili 25, 2026, katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar. Ibenge amebainisha kuwa timu yake ilianza mchezo kwa kusuasua kama walikuwa wanacheza mechi ya kirafiki, hali iliyowapa wapinzani wao upenyo wa kutawala mchezo mapema na hatimaye kuiondoa Azam FC kwenye kinyang’anyiro hicho. Akichambua makosa ya kiufundi, kocha huyo raia wa DR Congo amesisitiza kuwa kushindwa kumiliki mipira ya “50/50” ndiko kulikogharimu matokeo ya timu yake, kwani katika soka la ushindani, ukishindwa kwenye mapambano hayo ni vigumu kuibuka na ushindi.
Katika kuelezea hali ya mchezo huo ambao ulikuwa na ushindani mkali wa “Dabi ya Dar es Salaam” visiwani Zanzibar, Florent Ibenge alinukuliwa akisema:
”Sijui ni nini kimetokea, tulianza mechi vibaya kama tunacheza mechi ya kirafiki, wenzetu walianza vizuri na walikuja kucheza nusu fainali. Tulipoteza mipira mingi ya 50/50, kama huwezi kushinda mipira ya 50/50 huwezi kushinda mechi.”
Hatua hii inaiacha Azam FC ikijipanga upya kwa ajili ya mashindano yanayofuata ya Ligi Kuu ya NBC, huku Yanga SC ikisubiri mshindi kati ya Simba SC na Mlandege FC katika fainali ya mashindano hayo adhimu ya Muungano.
