KATIKA msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ushindani hauishii kwenye ufungaji wa mabao pekee, bali umehamia pia kwenye ubunifu wa pasi za mwisho (assist), ambapo nyota kadhaa wameibuka na kuonesha uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za mabao.
Miongoni mwa majina yanayotajwa zaidi ni Elie Mpanzu wa Simba, Feisal Salum maarufu kama Fei Toto wa Azam FC, pamoja na Duke Abuye wa Yanga. Wachezaji hawa wamekuwa na mchango mkubwa ndani ya timu zao, wakionesha ubora wa hali ya juu katika kutengeneza mabao.
Leo, mbali na ushindani wa kusaka alama tatu katika Mzizima Derby kati ya Azam FC na Simba, macho ya mashabiki pia yataelekezwa kwenye vita ya nani ataongoza kwa assist kati ya Mpanzu na Fei Toto.
Azam FC wanakuwa wenyeji wa Simba katika dimba la Azam Complex, Chamazi, huku kila timu ikihitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi.
Mpanzu, kiungo mshambuliaji wa Simba, ameendelea kuwa mhimili muhimu katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo. Utulivu wake akiwa na mpira pamoja na uwezo wa kuona nafasi mapema, umeifanya Simba kuwa hatari zaidi kila inaposhambulia.
Kwa upande wa Azam FC, Fei Toto ameendelea kuthibitisha ubora wake kama mmoja wa viungo bora nchini. Uzoefu wake mkubwa unamwezesha kutawala kiungo na kuunganisha timu kwa ufanisi, huku pasi zake za mwisho zikiwa silaha muhimu kwa washambuliaji wa Azam kufunga mabao.
Naye Duke Abuye wa Yanga amejiweka kwenye ramani ya ushindani huu kutokana na uwezo wake wa kupenyeza mipira hatari katika eneo la mwisho. Kasi yake pamoja na ubunifu vinamfanya kuwa tishio kwa mabeki wa timu pinzani kila anapokuwa uwanjani.
Ushindani wa nyota hawa watatu umeongeza ladha ya ligi, kila mmoja akipambana kuonesha ubora wake katika kila mechi. Mashabiki nao wamekuwa wakifuatilia kwa karibu kuona nani ataibuka kinara wa assist ifikapo mwisho wa msimu.
Hadi sasa, wachezaji hawa wanalingana kwa idadi ya pasi za mwisho, kila mmoja akiwa na assist tano. Hata hivyo, macho yote yako kwa Mpanzu na Fei Toto katika mchezo wa leo, ambapo mmoja wao ana nafasi ya kumpiku mwenzake na kuchukua uongozi.
Kwa mwendo huu, vita vya assist vinaonekana kuwa vikali zaidi kuliko ilivyotarajiwa, na bila shaka vitaendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa soka nchini.
