MIANO: KINDA MTANZANIA ALAMBA DILI NONO ULAYA

miano
Kinda wa kimataifa wa Tanzania, Miano Danilo van den Bos (22), amepiga hatua kubwa katika soka la kulipwa baada ya kujiunga na klabu ya FK Panevėžys inayoshiriki Ligi Kuu ya Lithuania (A Lyga). Huu unakuwa mkataba wake wa kwanza wa soka la kulipwa kwa beki huyo wa kati ambaye pia anaweza kucheza kama beki wa kulia na kiungo mkabaji, akitokea klabu ya FC Eindhoven ya Uholanzi.
​FK Panevėžys ni miongoni mwa klabu imara nchini Lithuania, ikiwa imetwaa ubingwa wa ligi hiyo mwaka 2023 na kushiriki michuano ya kukufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) hivi karibuni. Miano , ambaye tayari amewahi kuitwa na kuichezea timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars)  katika michuano ya AFCON na michezo ya kirafiki, anatarajiwa kuimarisha safu ya ulinzi ya klabu hiyo yenye maskani yake katika mji wa Panevėžys.
​Uhamisho huu unatazamwa kama fursa muhimu kwa mchezaji huyo mwenye asili ya Kitanzania na Kiholanzi kuonyesha uwezo wake katika jukwaa la soka la Ulaya na kuendelea kulinda nafasi yake kikosini Taifa Stars.
Mashabiki wa soka nchini Tanzania wamempokea kwa furaha mlinzi huyo anayejiamini akiwa na mpira, wakitegemea kuwa uzoefu atakaoupata Lithuania utakuwa na faida kubwa kwa timu ya taifa kuelekea kufuzu Kombe la Dunia 2026.