Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kesho Agosti 9 2025 inatarajiwa kucheza mchezo wa Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN 2024). Huo utakuwa ni mchezo wa tatu kwa Tanzania. Ni Tanzania vs Madagascar CHAN 2024 Uwanja wa Mkapa.
Mechi mbili zilizopita Tanzania ilipata ushindi kwa kuvuna pointi sita muhimu. Inatarajiwa kukutana na upinzani mkubwa kutoka kwa Madagascar. Timu hizi zote mbili zipo Kundi B ambalo vinara ni Tanzania.
Hemed Suleman Kocha Mkuu wa Tanzania amesema kuwa kila mchezo ni muhimu. Kocha huyo alibainisha kuwa hakuna timu ambayo haifikirii kupata ushindi. Licha ya yote hayo kocha huyo aliweka wazi kuwa ambao wanahitaji ni ushindi.
“Tuna kazi kubwa kwenye mechi zetu ambazo tunacheza. Maandalizi yapo vizuri hasa ukizingatia kwamba tulikuwa na kambi imara. Licha ya kwamba tumepata ushindi kwenye mechi zetu zilizopita bado tuna kazi kwa ajili ya mchezo wetu ujao,”.
Katika mechi mbili Tanzania ilifunga jumla ya mabao matatu, inaongoza kundi B ikiwa na pointi 6 kibindoni baada ya kucheza mechi zote Uwanja wa Mkapa.