Mayele Aendelea Kupambana na Ukame wa Mabao Pyramids FC
Hali bado ni tete huko Misri ambako mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Fiston Mayele, anaendelea kukabiliwa na ukame wa mabao akiwa na Pyramids FC. Licha ya timu yake kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ceramica Cleopatra katika Ligi Kuu ya Misri, nyota huyo alishindwa tena kufumania nyavu.
Ushindi huo umeifanya Pyramids FC kufikisha pointi 34 na kujikita nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi. Hata hivyo, kwa upande wa Mayele, mchezo huo umeongeza idadi ya mechi alizocheza bila kufunga kufikia 21 mfululizo katika mashindano tofauti.
Tangu alipofunga mara ya mwisho Oktoba 21 mwaka jana dhidi ya Pharco, Mayele hajatikisa nyavu katika ngazi ya klabu wala timu ya taifa. Katika michezo hiyo 21, mechi 15 ni za klabu na sita ni za timu ya taifa.
Ukame huo unakuja katika kipindi ambacho mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 31 anaelekea mwisho wa mkataba wake na Pyramids FC utakaomalizika Juni 30, 2026. Hali hiyo inaweza kuathiri mipango yake ya baadaye, hasa ikizingatiwa kuwa aliwahi kuhitajika na Al Ittifaq ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia kabla ya klabu yake kugoma kumuachia.
Msimu uliopita ulikuwa wa mafanikio kwa Mayele. Alifunga mabao sita katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kuisaidia Pyramids FC kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza. Aidha, alifunga mabao matatu katika mashindano ya FIFA ya klabu za Asia, Afrika na Oceania, akiongoza timu hiyo kuongeza ubingwa mwingine.
Tangu ajiunge na Pyramids FC Julai 30, 2023 akitokea Yanga SC, Mayele ameifungia klabu hiyo mabao 49 katika michezo 112. Takwimu hizo zinaonyesha mchango wake, licha ya changamoto ya sasa.
Kwa sasa, macho yote yataelekezwa kwake kuona kama ataweza kuvunja ukame huo na kurejea katika makali yake, huku Pyramids FC ikiendelea kupambana kusalia katika nafasi za juu za Ligi Kuu ya Misri.



