SIMBA RASMI YAREJEA KAMBINI KUJIANDAA, MIPANGO NI MIKUBWA SASA

simba

KIKOSI cha Simba SC kimeanza rasmi maandalizi yake leo  Jumapili, Januari 11, 2026 uwanja wa Mo Simba Arena, kikielekeza nguvu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance de Tunis.

Hatua hiyo inakuja baada ya mapumziko mafupi, huku benchi la ufundi likilenga kurejesha ushindani na umakini wa wachezaji kabla ya mechi hizo mbili muhimu.

Mchezo wa kwanza wa hatua hiyo unatarajiwa kuchezwa Januari 24, 2026, ambapo Simba itakuwa ugenini nchini Tunisia.

Mechi hiyo inatajwa kuwa ngumu kutokana na uzoefu na rekodi ya Esperance katika michuano ya kimataifa, jambo linalowafanya Wekundu wa Msimbazi kujiandaa kwa umakini mkubwa.

Katika mazoezi hayo, kocha Steve Barker na wasaidizi wake wanatarajiwa kuweka mkazo kwenye uimara wa safu ya ulinzi, kasi ya mashambulizi na matumizi sahihi ya nafasi.

Lengo ni kuhakikisha kikosi kinakuwa imara kimwili na kiakili kabla ya safari ya kuelekea Tunis.

Baada ya mechi ya kwanza, Simba itarejea nyumbani kujiandaa na mchezo wa marudiano utakaochezwa Januari 30, 2026, Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Uwanja wa nyumbani unatajwa kuwa silaha muhimu kwa Simba, huku mashabiki wakitarajiwa kujitokeza kwa wingi kuisukuma timu yao.

Viongozi wa klabu wameeleza imani yao kwa kikosi walichonacho, wakisisitiza kuwa maandalizi ya mapema ni sehemu ya mkakati wa kufikia malengo makubwa msimu huu.

Wamewataka wachezaji kuonyesha nidhamu, kujituma na kupigania nembo ya klabu uwanjani.

Kurejea kwa Simba mazoezini ni ishara ya dhamira yao ya kufanya vizuri katika michezo ya Ligi ya MabingwaAfrika huku  Mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona matokeo ya maandalizi hayo, wakitarajia timu yao kupigana kwa nguvu na kuandika historia mpya barani Afrika.