KUELEKEA mchezo wa Mzizima Derby, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameweka wazi kuwa ana kazi kubwa ya kuiboresha safu ya ushambuliaji ya kikosi chake, akiwataka washambuliaji wake kuwa watulivu zaidi wanapofika katika eneo la umaliziaji.
Barker aliyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa dakika 90 za mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambapo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
Licha ya ushindi huo muhimu, kocha huyo alieleza kuridhishwa na kiwango cha jumla cha timu yake, lakini hakusita kubainisha mapungufu yaliyojitokeza, hususan kupoteza mipira mara kwa mara na kushindwa kutumia vyema nafasi walizozipata.
Safu ya ushambuliaji ya Simba, inayoundwa na Selemani Mwalimu, Anicet Oura, Libasse Gueye pamoja na Neo Maema, sasa imepewa jukumu la kuhakikisha inakuwa makini zaidi mbele ya lango, hasa katika michezo ijayo yenye ushindani mkubwa.
Barker amesema changamoto hiyo ilionekana zaidi katika kipindi cha kwanza, ambapo licha ya kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, washambuliaji walikosa utulivu wa mwisho ulioweza kuzaa mabao zaidi.
“Wachezaji wamepambana na kufanikisha kupata alama tatu, lakini bado nina kazi ya kurekebisha maeneo hayo. Kipindi cha kwanza tulitengeneza nafasi nyingi ambazo kwa utulivu zaidi tungeweza kufunga mabao manne au matano,” amesema Barker.
Amesisitiza uwa ushindi huo ni chachu ya maandalizi ya michezo ijayo, huku akiahidi kuendelea kukinoa kikosi chake ili kuhakikisha kinakuwa imara katika kila idara.
Barker ameongeza kuwa baada ya mchezo huo, macho yao sasa yanaelekezwa kwenye pambano lijalo dhidi ya Azam FC, akisisitiza umuhimu wa kuibuka na ushindi ili kuendelea kujiweka kwenye nafasi nzuri katika mbio za ubingwa.
