WAKATI mzunguko wa 21 wa Ligi Kuu Zanzibar ukiendelea jana Alhamisi Aprili 2, 2026 baada ya kusimama kwa siku tatu, timu ya Junguni bado haijapata kocha mkuu wa kumalizia mechi zilizosalia.
Hayo yameelezwa na meneja wa timu hiyo, Shariff Omar Ramadhan wakati akizungumza na Mwanaspoti, akisema baada ya kujiuzulu kwa kocha mkuu, Mustafa Hassan Suleiman, bado haijapata mwingine.
Amesema wametafuta kocha wa mpito kwa lengo la kusimamia mechi mbili za mwanzo, huku timu ikiendelea kutafuta kocha mpya kuongeza nguvu ili isishuke. “Bado timu haijapata kocha rasmi wa kuisimamia lakini tunaye wa mpito ambaye ataisaidia kuiongoza timu hiyo kwa michezo miwili ya mwanzo tukiendelea kutafuta mwingine,” amesema.
Timu hiyo ilishuka dimbani jana Alhamisi kwenye Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani Pemba kucheza dhidi ya Uhamiaji, katika mwendelezo wa ligi hiyo.
Junguni United kabla ya janailikuwa nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi, imevuna pointi 10 kati ya michezo 20 iliyocheza huku ikifungwa mabao 48 na kufunga mabao 16.
Huu ni msimu wa pili kushiriki kwenye Ligi Kuu Zanzibar tangu ilipopata nafasi ya kupanda daraja msimu wa 2024-2025 kutokea huko Pemba.
