Home KITAIFA BARKER AWEKA WAZI SIRI YA HOFU, KABLA YA DERBY

BARKER AWEKA WAZI SIRI YA HOFU, KABLA YA DERBY

0
20

KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameweka wazi kuwa ubora wa viwanja vinavyotumika katika mechi za Ligi Kuu Bara ndiyo jambo linalompa wasiwasi mkubwa kwa sasa, hasa katika kipindi hiki ambacho timu yake inaelekea kwenye michezo muhimu.

Barker amesema hali ya baadhi ya viwanja inampa hofu kuhusu usalama wa wachezaji wake, kuwa jambo la msingi kwake ni kuhakikisha kikosi chake kinamaliza mechi kikiwa salama bila majeraha, hususan kuelekea michezo mikubwa ikiwemo Kariakoo Derby.

Ameeleza kuwa viwanja vyenye mashimo au nyasi zisizo katika hali nzuri vinaweza kusababisha madhara makubwa kwa wachezaji, hasa wanapokutana na timu zinazocheza soka la nguvu.

“Nazingira hayo humuweka mchezaji katika hatari ya kuumia kirahisi, Ukiniuliza kitu gani kinachonipa presha kwa sasa ni ubora wa viwanja.

Sitamani mchezaji wangu yeyote apate jeraha. Kiwanja chenye mashimo au nyasi mbovu kinaweza kusababisha maumivu na kuathiri mipango yetu,” amesema Barker.

Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo, kocha huyo ameonyesha imani kubwa kwa kikosi chake amesisitiza kuwa lengo la Simba ni kuhakikisha wanapambana na kubeba alama tatu katika kila mchezo.

Amesema wachezaji watakaopangwa lazima wawe fiti, wafuate maelekezo ya benchi la ufundi na kucheza kwa nidhamu na umakini mkubwa.

Barker ameongeza kuwa ushindani wa ligi ni mkubwa na mechi zijazo zitakuwa ngumu, lakini anaamini wachezaji wake wanafahamu thamani ya jezi wanayoivaa na wajibu wao kwa mashabiki na klabu kwa ujumla.

Kwa mtazamo wake, licha ya presha ya ushindani na changamoto za miundombinu, Simba itaendelea kupambana kufikia malengo yake, huku akitanguliza usalama wa wachezaji kama kipaumbele cha kwanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here