MWENYEKITI wa Simba, Muhtaza Mangungu, amesema uongozi wa klabu hiyo umepokea rasmi maboresho ya Katiba kutoka Serikalini na tayari umeanza kuyafanyia kazi kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi.
Kauli hiyo imekuja kufuatia hatua ya Msajili wa Vyama vya Michezo kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuikabidhi Simba Katiba yao iliyofanyiwa marekebisho, huku wakisisitiza klabu kuendelea na mchakato huo kama ilivyoelekezwa.
Mangungu ameeleza kuwa uongozi umepokea maelekezo hayo na unahitaji muda wa kuyapitia na kuyatekeleza kwa umakini, ili kuhakikisha kila kipengele kinafanyiwa kazi kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa ndani ya Katiba hiyo pamoja na miongozo ya kisheria.
Amesisitiza kuwa mchakato wa mabadiliko ndani ya klabu si jambo dogo, kwani unagusa mamlaka zaidi ya moja za Serikali, hali inayohitaji umakini na uratibu wa kina.
“Kuna eneo linalosimamiwa na Wizara ya Michezo, kuna eneo linalosimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria, pia linalosimamiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara,” amesema Mangungu, akibainisha kuwa kila hatua lazima izingatie matakwa ya kisheria.
Ameongeza kuwa mchakato huo ulianza muda mrefu, hivyo utekelezaji wake unahitaji subira na kufuata taratibu zote za kisheria ili kuhakikisha mageuzi hayo yanafanyika kwa usahihi na kwa manufaa ya klabu pamoja na wanachama wake.