BAADA ya wimbi la wachezaji wa Namungo kuzidi kukosa penalti katika mechi za Ligi Kuu Bara msimu huu, kocha wa kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, Juma Mgunda amesema hakuna mtu wa moja kwa moja wa kupiga isipokuwa aliyekuwa na utayari.
Kauli ya Mgunda inajiri baada ya Cyprian Kipenye kukosa penalti moja kati ya mbili ilizopiga juzi katika kichapo cha mabao 3-2, dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Akizungumza na Soka la Bongo, Mgunda amesema upigaji wa penalti hauna ufundi na ni utayari wa mchezaji mwenyewe, isipokuwa suala hilo kwa sasa anaendelea kulifanyia kazi ya kuwaandaa kisaikolojia, ili kutumia nafasi muhimu wanazopata uwanjani.
“Labda kwa sasa tungekuwa tunazungumza mechi iliisha kwa sare ya mabao 3-3, lakini kukosa kwetu penalti ikatugharimu, ni suala la saikolojia tu kwa mchezaji anayepiga siku husika kwa sababu hakuna ufundi wowote kwenye hilo,” amesema Mgunda, straika wa zamani.
Katika mechi hiyo, zilipigwa penalti tatu ambazo mbili alipiga Cyprian Kipenye katika dakika ya 39 na kufunga, kabla ya nyota huyo kukosa nyingine ya dakika ya 71, ikiwa ni dakika moja tu kabla ya George Mpole kuifungia Tanzania Prisons bao katika dakika ya 72.
Mabao ya Prisons yalifungwa na Lambert Sabyanka, George Mpole na Oscar Mwajanga, ikiwa ni ushindi wa kwanza kwa timu hiyo tangu Oktoba 21, 2025, ilipoifunga Mbeya City 2-1, huku pia bao jingine moja la Namungo likifungwa na Fabrice Ngoy.
Namungo ndio timu inayoongoza hadi sasa kupiga penalti nyingi msimu huu katika Ligi Kuu Bara, ambapo kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, kimepiga tano, huku kati ya hizo zimepigwa na nyota watatu tofauti na kupata mbili na kukosa tatu.
Penalti nne zimepigwa na nyota wawili na kila mmoja amefunga moja na kukosa pia moja, ambao ni Mkongomani Fabrice Ngoy mwenye mabao saba katika kikosi hicho, huku mwingine aliyefunga na kukosa ni Cyprian Kipenye aliyefunga mabao matatu.
Nyota mwingine aliyekosa penalti ambaye ni wa kwanza kabisa katika kikosi hicho ni Lucas Kikoti, wakati wa mechi ya timu hiyo dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, iliyoisha kwa sare ya kufungana kwa bao 1-1, Novemba 9, 2025.