KOCHA YANGA ATANGAZA KUONDOKA RASMI

Kocha Msaidizi wa Yanga SC, Matthew Silva, ametangaza rasmi kuondoka klabuni hapo kupitia waraka mrefu wa shukrani kwa viongozi, wachezaji na mashabiki wa Wananchi.
Kuondoka kwake kunatajwa kuhusishwa na mabadiliko ya benchi la ufundi kufuatia ujio wa Kocha Mkuu mpya Manqoba Mngqithi, pamoja na kupata fursa mpya ya kazi katika moja ya klabu za Ukanda wa Uarabuni.
Katika ujumbe wake wa kuaga, Silva amesema anaondoka akiwa ametimiza malengo yote aliyojiwekea tangu alipojiunga na Yanga.”Ninaondoka Yanga kwa namna ambavyo siku zote nilikuwa nikiota.
Lengo langu lilikuwa kuondoka nikiwa mtu mwenye utu, mchapakazi, mwenye kujitolea na mtaalamu wa kweli. Kwa furaha kubwa, lengo hilo limetimia.”
Silva ameondoka akiwa sehemu ya benchi la ufundi lililoisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tano mfululizo, akiiacha klabu ikiwa kwenye kipindi cha mabadiliko kuelekea msimu mpya.






