MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kwa kuwataka kuwa watulivu licha ya mwenendo wa hivi karibuni katika msimamo wa ligi.
Akizungumza kuhusu hali ya ushindani katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Ahmed amesema mashabiki hawapaswi kuchukulia kwa hofu tofauti ya alama iliyoanza kujitokeza, kuwa msimamo wa ligi hubadilika kwa kasi kubwa kama ilivyo katika masoko ya fedha.
“Dola inaweza kuwa Sh 2,560 asubuhi, ukienda jioni ukakuta Sh 2,480. Hivyo ndivyo ilivyo ligi,” amefafanua Ahmed, amesisitiza kuwa mabadiliko ya nafasi kwenye msimamo ni jambo la kawaida.
Ameongeza kuwa ingawa pengo la alama kati ya Simba na wapinzani wao limeongezeka kutoka alama moja hadi tano, hali hiyo haina haja ya kuwatia hofu mashabiki, kwani bado ni mapema katika mbio za ubingwa.
Kwa kujiamini, Ahmed amesema tofauti hiyo ni ya muda na itapungua tena hivi karibuni, akisisitiza kuwa malengo yao bado yapo palepale.
“Itaendelea kubadilika. Itakuja kuwa alama moja tena na Simba kukaa pale kileleni. Hilo ndilo tunalolifanyia kazi,” amesema.
Amewataka pia Wanasimba kuwa wavumilivu na kuendelea kuiamini timu yao wakati huu ambao ushindani umeongezeka.
“Wanasimba wasifedheheshwe. Sisi kama uongozi na benchi la ufundi tunajua namna ya kupunguza hizo alama,” ameongeza.
Ahmed amehitimisha kwa kuwahakikishia mashabiki kuwa mipango ya klabu ipo imara na inalenga kuhakikisha Simba inarejea kileleni mwa msimamo wa ligi.
Kauli hiyo inakuja wakati Simba ikiendelea na juhudi za kupunguza mwanya wa alama na kurejesha presha katika mbio za ubingwa wa msimu huu.
