UONGOZI wa klabu ya Simba SC umeweka wazi hali ya wachezaji wake waliopo majeruhi, huku beki Wilson Nangu akitarajiwa kurejea uwanjani Julai mwaka huu baada ya kuendelea na matibabu.
Akizungumza kuhusu hali ya kikosi, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema wachezaji wote walioumia wanaendelea na matibabu yao chini ya uangalizi wa madaktari wa timu, wakifuata maelekezo maalum ili kuhakikisha wanarejea wakiwa katika hali nzuri.
Alifafanua kuwa Nangu alifanyiwa upasuaji baada ya kupata majeraha makubwa na kwa sasa amewekewa P.O.P, hatua ambayo ni sehemu ya mchakato wa matibabu yake.
Baada ya hapo atawekewa bao maalum ambalo atalivaa kwa muda hadi pale atakapokuwa tayari kuanza mazoezi tena.
Ahmed amesema kwa sasa mchezaji huyo amerudi nyumbani kwao Boma Ng’ombe, Kilimanjaro kwa ajili ya kupata utulivu na kuendelea na hatua za kupona.
“Ripoti za madaktari zikionyesha kuwa anaweza kuanza mazoezi mwezi Julai endapo maendeleo yake yataendelea kuwa mazuri,” amessma.
Mbali na Nangu, Ahmed ameongeza kuwa wachezaji wengine wanaosumbuliwa na majeraha ni pamoja na Abdulrazack Hamza, Moussa Camara na Yakubu Suleiman ambao nao bado wanaendelea na matibabu na wanatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa muda hadi watakapopata nafuu kamili.
Amesema uongozi wa Simba umeendelea kuwahakikishia mashabiki kuwa unafuatilia kwa karibu maendeleo ya wachezaji hao ili kuhakikisha wanarejea uwanjani wakiwa tayari kusaidia timu kufikia malengo yake ya msimu.
