KUELEKEA mchezo wa kesho wa Der es Salaam Derby wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kocha mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, Amesema kuwa timu yake inakutana na changamoto kubwa dhidi ya wachezaji wenye viwango vya juu.
Amesema kuwa watakutana na timu ngumu zaidi kwenye ligi hii, ambayo imejipanga vyema kwa mechi hiyo muhimu.
“Timu yao ni imara sana, hasa ukizingatia ufanisi wao kwenye mashindano ya kimataifa. Tulicheza nao kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi, na nadhani wanapokuja kesho watakuwa wamejipanga vyema zaidi,” amesema Pedro.
Kesho, Yanga wanakabiliana na Azam FC katika mchezo wa nyumbani, utakaochezwa katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ambapo wanatafuta pointi tatu muhimu.
Kocha Goncalves ameeleza kuwa kucheza kwenye uwanja wa Mkapa ni changamoto mpya kwa timu yake, kwani ni mara ya kwanza tangu awe kocha wa Yanga.
“Kucheza uwanja wa Mkapa ni fursa nzuri sana kwetu. Uwanja huu ni mzuri, na tumejiandaa vyema ili kupata matokeo mazuri. Hakika kuna changamoto ndogo ndogo, hasa baada ya mchezo uliopita na safari nzima.
Wachezaji watakabiliana na uchovu, lakini tumepata muda wa kufanya maandalizi ya kuweka miili sawa tayari kwa mapambano,” amesema Pedro.
Kocha huyo pia amesisitiza umuhimu wa wachezaji kuwa na uelewa wa kimbinu, hasa wanapocheza katika viwanja tofauti.
“Changamoto kubwa ni kucheza katika mazingira tofauti, unaweza kucheza kwenye uwanja mbaya au mzuri. Ni lazima wachezaji wawe na ufahamu mkubwa wa kimbinu ili kukabiliana na vikwazo vya viwanja,” ameongeza.
“Wachezaji wangu wanafanya vizuri sana. Tokea nimeingia Tanzania, nimepata sare moja tu. Kwa kifupi, nina timu nzuri inayoweza kukabiliana na timu yoyote bila wasiwasi.
“Ninaposema Azam ni bora, haimaanishi kuwa tunaenda kwa hofu. Tunajiamini, tuna timu bora, sisi ni Yanga. Tunawaheshimu, lakini tutacheza kwa kujituma na kwa nidhamu kubwa,”amesema kocha huyo.
