Ruka hadi maudhui
SOKALEO

Mtazamo wa Ali Kamwe Kuhusu Samatta Kurejea Taifa Stars

Chikao
Mtazamo wa Ali Kamwe Kuhusu Samatta Kurejea Taifa Stars

Msemaji wa Yanga SC, Ali Kamwe, ametoa mtazamo wake kuhusu mjadala wa kurejea kwa Mbwana Ally Samatta katika kikosi cha Taifa Stars, akisema uamuzi wa mshambuliaji huyo kujitenga na timu ya taifa ulitokana kwa kiasi kikubwa na hasira zilizochochewa na namna alivyokuwa akitendewa na baadhi ya mashabiki na wadau wa soka nchini.

Kamwe amesema Watanzania wamechangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo kwa kushindwa kumthamini Samatta kwa kiwango anachostahili, akisisitiza kuwa mchezaji huyo ni miongoni mwa alama muhimu za soka la Tanzania kutokana na mchango wake kwa taifa.

Akizungumzia mabadiliko ya mtazamo kutoka kwa baadhi ya mashabiki, Kamwe amekosoa hali ambapo Samatta aliwahi kutajwa kuwa amefikia umri wa kupisha kizazi kipya, lakini baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 2-0 dhidi ya Guinea-Bissau, baadhi ya watu wakaanza kuitaka kurejea kwake katika timu.

Kwa mujibu wa Kamwe, Samatta bado ana uwezo wa kuisaidia timu ya taifa, akitolea mfano wa kuendelea kwake kufanya vizuri na kufunga mabao katika soka la Ufaransa.

“Kwa aliyoyafanya Samatta kwenye nchi hii, sio mchezaji wa kuagwa Instagram kwamba Samatta kwa heri. Anatakiwa arudi kwenye pitch tucheze mechi za AFCON pamoja naye,” alisema Kamwe.

Kamwe amemtaka Samatta kupunguza hasira na kufikiria kurejea katika kikosi cha Taifa Stars, hasa kwa kuzingatia kuwa Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Fainali za AFCON 2027. Kwa mtazamo wake, kurejea kwa Samatta kungempa nafasi ya kuhitimisha safari yake ya timu ya taifa akiwa uwanjani na kupata heshima kutoka kwa Watanzania.

Hata hivyo, Kamwe amesisitiza kuwa kurejea kwa wachezaji wenye uzoefu kama Samatta pamoja na mlinda mlango Aishi Manula hakupaswi kutafsiriwa kwamba wao ndio suluhisho la kila changamoto ya timu ya taifa.

Badala yake, amesema uwepo wao unapaswa kuonekana kama nyongeza ya uzoefu, ubora na thamani ndani ya kikosi cha Taifa Stars.

Shiriki:

Habari Zinazohusiana

Zaidi →

Kocha wa Simba Steve Barker Awasha Moto Mpya

YAMAL: Afikisha mchango wa mabao 20 ndani ya mechi 13