Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, amezusha mjadala mzito mitandaoni baada ya kurusha kijembe kizito kwa mahasimu wao wa jadi, Young Africans SC, kuelekea hatua za fainali za mashindano ya kombe la ndani. Ahmed Ally ameonekana kujiamini kupitiliza huku akidai kuwa walikuwa na hamu kubwa ya kukutana na Yanga kwani wamewasoma na kuwaona ni timu ya kawaida sana msimu huu.
Ahmed Ally amefunguka bila uoga akisema:-”Tulimtaka sana Yanga kwasababu ingekuwa Fainali nyepesi sana kwetu. Yanga haijawahi kutufunga kwenye kombe la CRDB. Msimu huu yeye ni mwepesi mno. Rekodi ya msimu huu, sisi ni bora sana kuliko yeye.”
Kauli hii ya kijeshi imekuja kama petroli kwenye moto, ikiamsha hisia za mashabiki wa pande zote mbili na kuongeza joto la upinzani wa jadi nchini. Ahmed Ally anatumia kete ya rekodi za nyuma za Kombe la CRDB (Federation Cup) kuonesha kuwa Simba ina jeuri ya kutosha mbele ya Yanga, huku akisisitiza kuwa ubora wao wa sasa unawapa jeuri ya kutwaa ubingwa kirahisi.
Je, unaona Ahmed Ally ana hoja ya msingi kuhusu Simba kuwa bora zaidi ya Yanga msimu huu kwenye Kombe la CRDB, au amewasokomezea maneno ya shombo Wananchi yatakayowatokea puani? Dondosha maoni yako hapa chini!