Ismail Mgunda: Sijuti Kujiunga na Simba SC, Ninaamini Tutashinda Derby

Mchezaji wa Simba SC, Ismail Mgunda, amesema hajuti kujiunga na klabu hiyo, akieleza kuwa amepata mbinu na uzoefu ambao hajawahi kuupata katika klabu nyingine, ikiwemo kipindi alipokuwa nchini Afrika Kusini.
Mgunda amesema amefurahishwa pia na namna alivyopokelewa na mashabiki wa Simba SC, akieleza kuwa licha ya kutarajia huenda akatengwa kama ilivyo katika baadhi ya nchi, amekuwa akipokea upendo na sapoti kutoka kwa mashabiki hao.
“Sijuti kujiunga na Simba SC, maana hata mbinu ninazopata hapa sijawahi kupata kwenye vilabu vingine, hata pale nilipokuwa Afrika Kusini,” amesema Mgunda.
Mchezaji huyo amesema anaamini ipo siku ataipa Simba SC ubingwa, akisisitiza kuwa ana deni kubwa kwa klabu hiyo na ana nia ya kufanya makubwa akiwa ndani ya timu hiyo.
Mgunda ajiamini kuelekea Kariakoo Derby
Akizungumzia mchezo wa Kariakoo Derby dhidi ya Yanga SC, Mgunda amesema hii itakuwa mara yake ya kwanza kushuhudia mchezo huo akiwa ndani ya kikosi cha Simba SC.
Mgunda amesema anaingia kwenye mchezo huo akiwa na matumaini makubwa kutokana na kiwango anachokiona kwenye mazoezi ya timu hiyo nchini Afrika Kusini.
“Binafsi naamini, kwa ninachokiona mazoezini Afrika Kusini, mchezo huu dhidi ya Yanga SC tutashinda. Nina asilimia 100 kwamba tunashinda,” amesema Mgunda.






