Ruka hadi maudhui
SOKALEO

CAF Yatafuta Mbadala wa Ku Host AFCON 2027

Chikao
CAF Yatafuta Mbadala wa Ku Host AFCON 2027

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeripotiwa kuanza kuchunguza uwezekano wa mipango mbadala kwa ajili ya AFCON 2027, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu kasi ya maandalizi katika nchi mwenyeji za Tanzania, Kenya na Uganda.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na vyombo mbalimbali vya habari, baadhi ya miundombinu muhimu ikiwemo viwanja, malazi na maandalizi mengine ya mashindano hayo bado inahitaji kukamilishwa kwa kasi ili kukidhi viwango vinavyotakiwa na CAF.

Ripoti kutoka gazeti la Ufaransa Le Monde zinadai kuwa CAF imewasiliana na baadhi ya nchi ili kuchunguza uwezekano wa kuwa na mpango wa dharura endapo Tanzania, Kenya na Uganda zitashindwa kukamilisha maandalizi kwa wakati.

Nchi zilizotajwa katika taarifa hizo ni Morocco, Algeria na Afrika Kusini, huku Côte d’Ivoire na Misri pia zikitajwa kama chaguo zinazoweza kuangaliwa.

Hata hivyo, taarifa hizi zinakuja licha ya kauli ya Rais wa CAF, Patrice Motsepe, aliyesema hivi karibuni kuwa hakuna mpango wa kuhamisha AFCON 2027 kutoka Tanzania, Kenya na Uganda.

Motsepe alisema CAF haina “Plan B” wala “Plan C”, huku akisisitiza kuwa maeneo ambayo bado yako nyuma katika maandalizi yanapaswa kuharakishwa na kukamilishwa kwa wakati.

CAF imesema itaendelea kufanya ukaguzi wa maendeleo ya maandalizi katika nchi hizo tatu. Motsepe pia anatarajiwa kurejea kwa ukaguzi mwingine mkubwa Januari 2027, ambao utakuwa muhimu katika kutathmini hali ya mwisho ya maandalizi.

Kwa sasa, AFCON 2027 bado imepangwa kufanyika Tanzania, Kenya na Uganda kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, na hakuna tangazo rasmi la CAF linalothibitisha kwamba uenyeji umehamishwa kwenda nchi nyingine.

Hivyo, kinachozungumziwa kwa sasa ni uwezekano wa mipango ya dharura, si uamuzi rasmi wa kuiondoa AFCON 2027 Afrika Mashariki.

Shiriki:

Habari Zinazohusiana

Zaidi →

Kocha wa Simba Steve Barker Awasha Moto Mpya

YAMAL: Afikisha mchango wa mabao 20 ndani ya mechi 13