Ruka hadi maudhui
SOKALEO

Serikali Yatoa Wito Kwa Klabu ya Simba Kutekeleza Katiba Mpya

Chikao
Serikali Yatoa Wito Kwa Klabu ya Simba Kutekeleza Katiba Mpya

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limetoa ufafanuzi kwa umma,wanachama na wadau wa Klabu ya Simba kuhusu utekelezaji wa Katiba ya Klabu hiyo iliyorekebishwa na kuidhinishwa tarehe 18 Februari, 2026.

Marekebisho hayo yalipitishwa na Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Klabu ya Simba tarehe 30 Novemba, 2025, na kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama na Vilabu vya Michezo kwa uchambuzi na kuidhinishwa kwa mujibu wa sheria na kanuni husika.

Baada ya uchambuzi wa kisheria, BMT kupitia Msajili wa Vyama na Vilabu vya Michezo iliidhinisha na kukabidhi rasmi Klabu ya Simba Katiba iliyorekebishwa tarehe 18 Februari, 2026 ili ianze kutumika.

Kwa msingi huo, Serikali inafafanua kuwa ilikamilisha wajibu wake wa kuidhinisha na kukabidhi Katiba hiyo. Kuanzia hapo, wajibu wa kutekeleza Katiba na kukamilisha mabadiliko yaliyopitishwa na wanachama ni wa Klabu ya Simba yenyewe.

Utekelezaji wa maamuzi yaliyomo katika Katiba hiyo haupaswi kufanywa na Serikali kwa niaba ya Klabu, kwa kuwa ni maamuzi yaliyofanywa na wanachama kupitia Mkutano Mkuu na kuidhinishwa kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, Serikali inatambua kuwa utekelezaji wa mabadiliko hayo unaweza kuibua masuala ya utaratibu unaohitaji ufafanuzi. Kwa hiyo, BMT na taasisi nyingine husika za Serikali ziko tayari kuipokea Klabu ya Simba kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa utaratibu pale inapohitajika, kwa mujibu wa mamlaka ya kila taasisi.

Hivyo, Serikali inatoa wito kwa Klabu ya Simba kutumia vyombo na taratibu zake halali kukamilisha utekelezaji wa Katiba iliyoidhinishwa, na kuwasilisha rasmi kwa mamlaka husika masuala yoyote yanayohitaji ufafanuzi.

Serikali itaendelea kutekeleza jukumu lake la kuendeleza sekta ya michezo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu, huku ikilenga maendeleo ya vilabu na sekta ya michezo kwa ujumla wake.

Ni matarajio ya Serikali kuwa masuala ya maendeleo ya michezo yataendelea kushughulikiwa kwa kuzingatia utulivu, uwazi, uwajibikaji maslahi ya wananchi na wapenzi wa michezo.

Shiriki:

Habari Zinazohusiana

Zaidi →

Kocha wa Simba Steve Barker Awasha Moto Mpya

YAMAL: Afikisha mchango wa mabao 20 ndani ya mechi 13