MPENJA: CHAMA ALIKUWA ANAOMBA MUNGU SANA ARUDI SIMBA

Mtangazaji na mchambuzi wa michezo Baraka Mpenja amefunguka kuhusu safari ya kurejea kwa kiungo mshambuliaji Clatous Chama ndani ya kikosi cha Simba SC, akieleza namna ambavyo nyota huyo alikuwa na hamu kubwa ya kuirudia timu hiyo licha ya baadhi ya mashabiki kuwa na mashaka juu ya uwezo wake.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Baraka amesema wakati Chama akitaka kurejea Simba akitokea Singida Black Stars, kulikuwa na mgawanyiko mkubwa miongoni mwa mashabiki wa Simba ambapo baadhi yao walikuwa hawaungi mkono kurejea kwake wakidai amezeeka na hawezi tena kucheza katika kiwango cha juu.
“Mimi Chama ni rafiki yangu sana na alipotaka kurudi Simba kutokea Singida, hata Wanasimba wenyewe waligawanyika, wengine wakawa hawamtaki wengine wanamtaka,” amesema Baraka Mpenja.
Ameongeza kuwa alimhoji Chama kuhusu maneno yaliyokuwa yanaendelea mitandaoni, ndipo kiungo huyo akamweleza kuwa kurejea Simba ilikuwa ndoto aliyokuwa akiisubiri kwa muda mrefu.
“Nilimuuliza, ‘Kaka wanasema umezeeka hautaweza,’ akaniambia, ‘Kaka nimeomba nafasi hii muda mrefu ya kurudi Simba, nimemuomba sana Mungu nataka nikaisaidie timu yangu,’” amesema Baraka.
Kauli hiyo imeendelea kuwavutia mashabiki wengi wa Simba, hasa baada ya Chama kuonyesha kiwango bora tangu kurejea kwake, ambapo ameendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu na tishio kubwa ndani ya kikosi hicho.






