SIMBA Queens imepeleka barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufungua kesi juu ya mchezaji wake, Aisha Mnunka ambaye hajarejea kambini hadi sasa.
Agosti, mwaka huu, Sokaleo ililiripoti kuwa mshambuliaji huyo wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Twiga Stars’ aliondoka kambini bila viongozi kufahamu chochote wakati timu hiyo ikijiandaa na michuano ya Cecafa.
Mbali na kutoroka, ilielezwa kwamba bosi mmoja wa timu ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara amemuahidi Nyota huyo kwamba akicheza timu yake atamnunulia gari, simu na nyumba ambavyo hadi sasa hajakabidhiwa na mawasiliano ya straika huyo hayapatikani.
Mnunka bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba Queens ambao unatamatika mwishoni mwa msimu huu. Akizungumza Meneja wa Simba, Selemani Makanya alisema nyota huyo hajawasili kambini na viongozi wame fungua kesi TFT.
“Tumeshapeleka barua TFF, tunasubiri kufuatiliwa wiki ijayo, bado ni mchezaji wetu na hadi sasa hatuna mawasiliano naye, simu yake ikipigwa haipatikani, hivyo huo ndio uamuzi wetu,” alisema Makanya.