KAMWE AWAPONGEZA COASTAL UNION KWA KULETA TIMU, DONGO HILI

ALI Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wapinzani wao Coastal Union wanahitaji pongezi kwa kuwa sio jambo rahisi kupeleka timu kukabiliana na Yanga.
Ujumbe huo ni kama dongo kimtindo kwa watani zao wa jadi Simba ambao Machi 8 2025 mchezo wao wa Kariakoo Dabi ulighairisha kutokana na kile ambacho Simba walieleza kuwa hawakupewa nafasi ya kufanya mazoezi ya mwisho Machi 7 kwa mujibu wa kanuni.
Malalamiko yao yalifika kwa Bodi ya Ligi Tanzania, (TPLB) ambao walikaa kikao na kutoa taarifa kuwa mchezo huo umeghairishwa na utapangiwa tarehe nyingine.
Machi 12 2025, Yanga ilikuwa na kibarua cha kusaka ushindi mbele ya Coastal Union ya Tanga ambao nao walikuwa wanasaka ushindi katika hatua ya 32 bora na mwisho ubao ukasoma Yanga 3-1 Coastal Union.
Mabao ya Maxi Nzengeli dakika ya 2 na 15 na Clement Mzize dakika ya 21 huku bao pekee la Coastal Union likifungwa na Miraji Abdallah dakika ya 18 kwa mguu wake wa kushoto akiwa nje ya 18.
“Tunawapongeza Coastal Union kwa kuleta timu uwanjani maana sio kazi rahisi kuleta timu ije kucheza na Yanga. Tumepata matokeo mazuri ya ushindi na ukizingatia kwamba sisi ni mabingwa watetezi hivyo tunasonga mbele mpaka hatua ya 16 bora kwa sasa.”
Simba Machi 11 walishuka Uwanja wa KMC Complex kumenyana na TMA Stars na mwisho ubao ukasoma Simba 3-0 TMA Stars, hivyo wababe wote wawili wametinga hatua ya 16 bora.