Jeraha Jipya la Neymar Lazua Gumzo Kisa Birthday ya Dada yake.

Nyota wa Timu ya Taifa ya Brazil na klabu ya Santos Neymar Jr alfajiri ya leo ameshindwa kucheza mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya Corinthians huko Brazil klabu yake ilipopoteza kwa 2-1 kutokana na maumivu anayoyasikia.
Akizungumza baada ya mchezo huo Neymar amesema “Kwa bahati mbaya nilihisi maumivu kwa wiki kadhaa sasa,nilitamani kuisaidia timu, tulifanya vipimo asubuhi lakini nilihisi maumivu tena” Neymar amefunguka hayo licha ya kutoweka wazi ni sehemu gani anapohisi maumivu.
Jambo hilo limezua gumzo huku baadhi ya watu wakihusisha majeraha ya nyota huyo na siku ya kusherekea kumbukumbu ya kuzaliwa ya dada yake Rafaella Santos siku ya kesho Machi 11.
Nyota huyo amekuwa na rekodi ya kuwa nje ya ‘program’ za timu anazozitumikia kila inapokaribia Machi 11 aidha kwa majeraha au kwa kadi ambayo itamfanya akose mchezo unaofuata tangu msimu wa 2014/15 ambapo alikuwa akizitumikia Barcelona na PSG.