KITAIFA

YANGA WATIA NENO JUU YA ‘FEI TOTO’, SAFARI SASA IMEIVA

Nyota wa Yanga, Max Nzengeli na Khalidy Aucho, wamejitokeza kumpongeza kiungo wa Azam FC na timu ya taifa ya Tanzania, Feisal Salum ‘Feitoto’, kwa uwezo wake mkubwa na kipaji kinachovutia kwenye soka la Tanzania.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Nzengeli alieleza kuwa Feitoto ni mchezaji wa kipekee nchini. “Kwa wachezaji wa ndani, Feitoto ni mmoja wa wachezaji bora. Anafahamu mpira, anaweza kucheza sehemu yoyote, na Watanzania wanapaswa kujivunia kipaji chake,” alisema Nzengeli.

Aidha, Nzengeli alimpongeza pia kiungo wa Simba, Awesu Awesu, akimtaja kuwa miongoni mwa wachezaji wenye uwezo mkubwa nchini.

Kwa upande wake, Khalidy Aucho, ambaye ni mchezaji wa kimataifa kutoka Uganda, alikiri kufurahishwa na kiwango cha Feitoto. “Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji, lakini kwangu Feitoto ni bora zaidi. Namfuatilia mara kwa mara anapocheza Azam FC, na uwezo wake ni wa hali ya juu,” alisema Aucho.

Feisal Salum ‘Feitoto’, ambaye alijiunga na Azam FC msimu uliopita kutoka Yanga, amejijengea heshima kama mmoja wa viungo mahiri nchini Tanzania. Kabla ya kujiunga na Yanga, alikuwa akikipiga na Singida United wakati wa ushiriki wao katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wachezaji wa soka na mashabiki wanamtaja Feitoto kama mfano wa kuigwa kwa bidii na mafanikio yake, akiwakilisha soka la Tanzania katika kiwango cha juu.

Related Articles

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button