SIMBA YAIVUTIA KASI TABORA UNITED

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa hesabu kubwa kwa sasa ni kupata matokeo mazuri dhidi ya Tabora United mchezo wao wa Ligi Kuu Bara inayodhaminiwa na NBC.
Ipo wazi kuwa Tabora United kwenye mechi zake zilizopita dhidi ya timu ambazo zipo ndani ya tatu bora ilipata matokeo kwa kukomba pointi tatu mazima ilikuwa dhidi ya Yanga kwa ushindi wa mabao 3-1 Uwanja wa Azam Complex dhidi ya Azam FC kwa ushindi wa mabao 2-1 Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wapo tayari kwa mchezo wao dhidi ya Tabora United na kikubwa ni kuona kwamba wanapata pointi tatu kutokana na umuhimu wa mchezo huo.
“Kwetu Simba kila mchezo ni muhimu na tunatambua kwamba Tabora United ilipata matokeo kwenye timu moja hivi ambao ni watani zetu wa jadi sasa tunakwenda kucheza kwa umakini kutafuta ushindi inawezekana na wachezaji wapo tayari.
“Ushindi kwenye mchezo wetu dhidi ya Kilimanjaro Wonders ni muhimu sana kwa kuwa umeongeza hali ya kujiamini kwa vijana hivyo tunakwenda kupambana na wapinzani wetu ambao wapo imara na kikubwa ni kuona tunapata pointi tatu muhimu.”
Kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids baada ya mechi 15 ni ushindi kwenye mechi 13, sare moja na kupoteza mchezo mmoja ndani ya ligi namba nne kwa ubora.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumapili ambayo itakuwa ni Februari 2 2025 saa 10:00 jioni, Tabora watakuwa nyumbani.