HIZI HAPA HESABU ZA RAMOVIC KUFUZU ZIPO SAWA
Kocha mkuu wa Yanga, Sead Ramovic amesema hadi sasa hesabu za timu hiyo kutinga Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zipo sawa baada ya kuifumua TP Mazembe kwa mabao 3-1 na kudai kipigo hicho ni kidogo kuliko nafasi walizotengeneza.
Ramovic, aliyepata ushindi wa kwanza CAF akiwa kocha wa Yanga, alisema kuimarika kwa wachezaji wakishika haraka na vizuri falsafa alizowapa zinampa imani wanaweza kushinda mbele ya Al Hilal wikiendi hii ugenini, kisha kurudi nyumbani kuifumua MC Alger Januari 18.
“Ni matokeo yaliyotupa imani kuwa, bado tunaweza kufanya kitu kufikia lengo la kutinga robo fainali, hii ilikuwa mechi kubwa tumeiamua kwa nguvu kubwa ya ubora wetu,” alisema Ramovic na kuongeza
“Tunahitaji kuendeleza matokeo kama haya katika mechi mbili zinazofuata, nafurahi namna wachezaji wanavyoendelea kuimarika, tunacheza mpira tunaotaka tuucheze kwa kumnyima mpinzani nafasi ya kupumua.”
Tunawaheshimu sana wapinzani wetu (Mazembe) lakini tulistahili ushindi mkubwa zaidi tungeweza kufunga mabao matano hadi sita kama tungeongeza umakini.“