HII HAPA HATMA YA YANGA KUFUZU ROBO FAINALI, WAKIFELI NDIO BADI TENA
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic, amesisitiza kuwa mechi dhidi ya TP Mazembe itakayochezwa Jumamosi, Januari 4, ndiyo itakayoamua mustakabali wa timu hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika. Ramovic amewataka mashabiki wa Yanga kuujaza uwanja kwa wingi ili kuipa timu yao nguvu ya ushindi.
Katika mechi hiyo ya marudiano, Yanga inahitaji ushindi wa lazima ili kuendeleza matumaini yao ya kufuzu robo fainali ya michuano hiyo. Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo ulimalizika kwa sare ya 1-1 jijini Lubumbashi, jambo ambalo linaifanya mechi ya Jumamosi kuwa na uzito wa pekee kwa timu zote mbili.
“Hatima ya kufuzu ipo mikononi mwetu. Tunajua mchezo hautakuwa rahisi kwa sababu TP Mazembe nao wanahitaji ushindi. Lakini tukiwa nyumbani na mashabiki wetu wakiwa nyuma yetu, tuna nafasi nzuri ya kupambana na kushinda,” alisema Ramovic.
Yanga, ambayo ipo nafasi ya mwisho katika Kundi A ikiwa na pointi moja pekee baada ya mechi tatu, inahitaji ushindi dhidi ya TP Mazembe ili kufikisha pointi nne na kujiweka kwenye nafasi ya kupigania nafasi ya kufuzu. Al Hilal wanaongoza kundi hilo wakiwa na pointi tisa, wakifuatiwa na MC Alger wenye pointi nne, huku Mazembe wakiwa na pointi mbili.
Ramovic ameongeza kuwa kikosi chake kinafanya maandalizi ya kina kuhakikisha wanapambana kwa mbinu na kufanikisha ushindi kwenye mchezo huo muhimu.
“Tumewasoma wapinzani wetu na tunaendelea kuboresha baadhi ya maeneo kwenye mazoezi. TP Mazembe ni timu yenye uzoefu, lakini nasi tuko tayari kwa changamoto hiyo,” alisema kocha huyo.
Ikiwa Yanga itashinda mchezo huo, itakuwa imepata nafasi ya kuendelea kupigania kufuzu kwa kushinda mechi mbili za mwisho dhidi ya MC Alger na Al Hilal.
Mashabiki wa Yanga wameombwa kujitokeza kwa wingi ili kuwapa wachezaji motisha ya kuibuka na ushindi kwenye mechi hii ya kihistoria.