TFF WAIBUKA NA JIPYA USAJILI WA MPANZU SIMBA….”WAMEZIDISHA WACHEZAJI WA KIGENI”
IMEBAKIA muda mchache tu kabla ya mashabiki na wanachama wa Simba kumuona staa wao Mkongomani, Elie Mpanzu uwanjani lakini Kocha Fadlu Davids ameweka wazi jinsi atakavyopindua mezani kwenye kikosi cha kwanza.
Ikumbukwe dirisha dogo la usajili litafunguliwa Desemba 15 na kufungwa Januari 15 muda ambao bado Simba itakuwa ikipambana kwa udi na uvumba kwenye Ligi ya ndani na michuano ya kimataifa ambako msimu wamepania kufika mbali na kuweka rekodi.
Mpanzu ambaye ana uzoefu mkubwa kwenye ligi za Afrika, alisaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Simba Septemba mwaka huu, huku akikadiriwa kuchukua jumla ya Sh782milioni ndani ya mkataba huo aliousaini mbele ya MO na msaidizi wake Salim Try Again.
Winga huyo alitua Simba akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake na AS Vita kumalizika na ambapo aliripotiwa kufanya majaribio ya klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji lakini mambo hayakwenda vizuri.
Mpanzu katika nafasi yake anacheza pamoja na Kibu Denis,Edwin Balua,Ladaki Chasambi na Joshua Mutale, ambao wote wamekuwa na rekodi za kucheza katika kikosi cha kocha Fadlu.
Kocha wa kikosi hicho, Fadlu David amezungumza na Mwanaspoti kuliambia kuwa anamsubiri kwa hamu Mpanzu na ambavyo anaweza akapangua safu ya ushambuliaji yake kutokana na ubora aliouonyesha mazoezini ndani ya kipindi kifupi.
Alisema kuwa anaweza kumtumia kama kiungo mshambuliaji na anaweza akatokea maeneo yote mawili ya pembeni, anaweza kucheza kama namba 10 lakini zaidi anauwezo mkubwa wa kufunga na kutengeneza nafasi.
“Mpanzu amechangamka ni mtu mwenye ushirikiano na mchango mkubwa kwenye timu, nasubiri kwa hamu aanze kazi, kwani imani yangu ni kubwa kutokana na kiwango bora alichokionyesha,”alisema Kocha huyo ambae mashabiki wa Simba wameanza kumuelewa na kumsifu mitandaoni.
“Kuwa na mchezaji mwenye uwezo wa kucheza maeneo mawili akitokea pembeni ni jambo zuri kwani anakupa vitu vingi Uwanjani naweza kumtegemea kama kiungo na hata winga.”
Aliongeza kuwa:”Shauku ya Mpanzu ni kufanya vizuri wakati wote namuona mazoezini anavyojituma kama anacheza mechi kubwa wachezaji wenzake ni mashahidi, nasubiri muda wake wa kucheza ufike ili aongeze ushindani ndani ya timu.”
TFF SASA
Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF Salum Madadi alisema kuwa, Mpanzu ataweza kuitumikia Simba mara baada ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa kwa kuwa ni mchezaji huru.
Lakini aliongeza kuwa, kabla ya Simba kuanza kumtumia watahitajika kumuondoa mchezaji mmoja kwenye usajili wao wa sasa. “Ataweza kucheza baada ya dirisha dogo kufunguliwa mwezi huu, lakini kuhusu idadi ya wachezaji wakigeni tayari walishakamilisha 12 wanaohitajika kikanuni ili kuingiza jina la Mpanzu.”
Awali iliripotiwa MO alinasa saini ya Mpanzu akiipiga bao Yanga kwa kumpa dau la Dola 200,000 (Sh543.3 milioni) kwa miaka miwili ambapo kila mwaka atachukua Dola 100,000 (272 millioni).
Hata hivyo baada ya kumsajili staa huyo hakuweza kucheza baada ya kuchelewa dirisha la usajili, ila Simba ikaona sio kesi ikaamua kumtangaza na kuweka wazi ataanza kucheza mzunguko wa pili.
Simba baada ya kucheza mechi mbili za kimataifa dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola kuifunga bao 1-0 nyumbani na kupoteza na CS Constantine ya Algeria kwa mabao 2-1 ugenini.
Simba iko kundi A katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya Makundi, itakuwa nyumbani Jumapili Desemba 15 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kukichapa dhidi ya SC Sfaxien ya Tunisia.
MSIKIE AHMEDY ALLY
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ahmedy Ally alisema kuwa, Mpanzu anasubiri usajili wake kuingizwa kwenye dirisha la usajili lijalo.
“Mechi yetu ijayo ya Shirikisho tutacheza na SC Sfaxien ya Tunisia hapa Dar kisha timu hizo zitakaporudiana ndio ataweza kucheza.
Michezo hiyo itachezwa Januari ambapo ataweza kuwa tayari, pia ITC yake ilishafika kilichobaki ni kukamilisha mchakato wa kikanuni kwa usajili wake kuingizwa kwenye mfumo.”